𝐆𝐀𝐕𝐀𝐍𝐀 𝐁𝐀𝐑𝐀𝐒𝐀 𝐀𝐄𝐋𝐄𝐊𝐄𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐖𝐀𝐙𝐈𝐑𝐈 𝐊𝐔𝐙𝐈𝐍𝐆𝐀𝐓𝐈𝐀 𝐌𝐈𝐑𝐀𝐃𝐈 𝐈𝐍𝐀𝐘𝐎𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐀
Gavana Mchapakazi FCPA Fernandes Barasa amelielekeza baraza lake la mawaziri kuzingatia miradi inayoendelea kukamilishwa ili kuzuia kukwama kwa miradi mipya wakati huu ambapo mgao wa kaunti unakisiwa kupungua kwa kiasi cha shilingi bilioni 20.
Gavana Barasa alikuwa akizungumza katika mkutano wa kufunga kikao cha Mpango wa Maendeleo wa Kaunti ya Kakamega (ADP) kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026, uliohudhuriwa pia na maafisa wakuu wa kiufundi.
Akizungumzia changamoto hii, Gavana Barasa ametilia mkazo hatua mbalimbali za kubana matumizi ya fedha nje ya mipango ya serikali, huku akihimiza kitengo cha Mapato ya Ndani kujizatiti katika ukusanyaji ushuru ili kufadhili miradi endelevu kulingana na manifesto yake.
Manifesto ya Gavana Barasa inajumuisha ajenda sita: Afya bora, ikihusisha ufunguzi wa vituo vya afya, usambazaji wa dawa na huduma za ambulensi, Maji na Usafi, inayojulikana kama “Amatsi Khumuliango,” Uzalishaji Mali na Uimarishaji Miundo msingi, ikiwemo ufunguzi wa viwanda; Usalama wa Chakula, ukijumuisha ugavi wa vyakula vya mifugo, Ruzuku ya pembejeo na mengineyo; Elimu bora, ikiwa ni pamoja na basari na udhamini wa elimu, unaojulikana kama Barasa Jamii; Huduma za jamii, pamoja na Uongozi bora.